Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

WIZARA YA ARDHI NA BENKI YA DUNIA ZALENGA KUANZISHA KITUO CHA UBUNIFU NA MAFUNZO YA TAARIFA ZA KIJIOGRAFIA (ZANZIBAR GEO-INNOVATION CENTER)

Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wanatarajia kuanzisha kituo cha kisasa kitakachosaidia katika masuala ya Ubunifu na mafunzo ya taarifa za kijiografia (Zanzibar Geo-Innovation Center)  ili kuibua wataalamu na wabunifu katika sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhandisi Dkt. Mngereza Mzee Miraji wakati akizungumza na Meneja msimamizi wa Ardhi na mipango miji kwa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Catalina Marulanda ofisini kwake Maisara, Unguja.

“Adhma ya Wizara katika kuanzisha kituo cha kisasa cha ubunifu na mafunzo ya taarifa za kijiografia (Geo-Innovation Center) itasaidia kuibua mambo mengi ikiwemo wataalam na wabunifu” Alisema Dkt Mngereza.

Kupitia kikao hicho viongozi hao wamezungumzia juu ya masuala yanayohusiana na ardhi pamoja na uwendelezaji wa sekta ya Makaazi.

Pia, wamejadili juu ya suala zima la ujenzi wa nyumba za kisasa za gharama nafuu ambazo zitawanufaisha wananchi wenye kipato cha chini hapa Zanzibar.

Kwa upande wake Meneja msimamizi wa Ardhi na mipango miji kwa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Catalina Marulanda ameonesha utayari wa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar katika kuanzisha kituo hicho.

Kikao hicho ni kikao cha mazungumzo ya awali ya uanzishwaji wa kituo cha Geo- Innovation Center na baadae itafatia kikao cha makubaliano na hatimae ujenzi wa kituo chenywe.

Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi imefungua milango yake katika kuimarisha uwekazaji Zanzibar katika sekta mbali mbali.
 
Imetolewa na Kitengo cha Habari. (WAMM).
Febuari 20, 2024.