Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

WAZIRI RAHMA KASSIM ALI AAHIDI KUPATIA UFUMBUZI MGOGORO WA ARDHI NDUNDUKE NDANI YA KIPINDI KIFUPI

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali amesema Wizara itaupatia ufumbuzi mgogoro wa Ardhi uliodumu kwa muda mrefu kwa wananchi wa Ndunduke  ili kuondosha sitomfahamu na hatimae kuwaruhusu wananchi kuendelea na harakati zao.

Mhe. Waziri Rahma Kassim Ali ameeleza hayo wakati alipofika katika eneo hilo la mgogoro liliopo Dole Wizlaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Mgaharibi.

Mhe. Waziri amezitaka pande zote zilizomo katika mgogoro hua kutotumia nguvu kwani Serikali italipatia ufumbuzi suala hilo ndani ya kipindi cha muda mfupi na kila mmoja atapata haki yake.

Aidha Mhe. Waziri Rahma  ameiagiza Kamisheni ya Ardhi mara baada ya mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi kulipima eneo hilo sambamba na kufanya utambuzi mara moja.

Katika kipindi hichi ambacho Wizara inakwenda kuupatia ufumbuzi mgogoro huo amewasisitiza wananchi hao kuendelea kutii agizo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya la kutoendelea na ujenzi wowote katika eneo hilo.

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A”Mhe. Suzan Peter Kunambi ameushukuru uongozi wa Wizara ya Ardhi na Makaazi kwa hatua ilioanza kuzichukua mara baada ya mgogoro huo kufikishwa katika Ofisi ya Mhe. Waziri.

Kwa upande Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu Mzee Haji Ali amesema Wizara itaenda kuunda timu ya watu kumi (10) itakayoshirikisha pande zote na kuanza kukaa vikao vyake ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (WAMM)
Febuari 18, 2024