Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe Rahma Kassim Ali amewatoa hofu wananchi wa Ndijani na Tunguu katika kazi ya tathmini

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe Rahma Kassim Ali amewatoa hofu wananchi wa Ndijani na Tunguu  katika kazi ya tathmini inayofanywa ndani ya maeneo hayo ambapo kila mwananchi atakaeathirka eneo lake atalipwa kwa mujibu wa thamani ya eneo au kipando chake.

Aliyasema hayo huko Ndijani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipokua akizungumza na wananchi wa maeneo hayo kufuatia baadhi ya wananchi kukataa kufanyiwa tathmini na kuondoa alama ambazo ziliwekwa na Serikali kitendo ambacho kinarudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo nchini.

Alifahamisha kuwa Serikali haina nia ya kumdhulumu mwananchi yoyote na inapopanga mipango yake hulenga katika kuwaletea wananchi huduma bora na sio vyenginevyo hivyo kwa sasa Serikali imeamua kuipanga ardhi yote ya Zanzibar ili wananchi waweze kufikiwa na huduma hizo kwa urahisi zikiwemo ujenzi wa barabara,Hospital,Pamoja na kuweko kwa Makaazi bora, hivyo wananchi hawana budi kutoa ushirikiano wa kutosha katika zoezi hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kati Marine Joe Thomasi amewaomba wananchi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwani kazi ya upimaji na ufanyaji tathmini ni hatua muhimu katika kuondokana na migogoro ya ardhi nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi Ndg.Muchi Juma Ameir amesema tathmini inafanywa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kisheria na unaangalia baada ya kupima ambapo kila kitu kinajulikana thamani yake.

Nao wananchi wa maeneo hayo wameiomba Serikali kuhakikisha tathmini  hiyo inaendana na hali halisi ya wakati uliopo kwa kulinganisha na maeneo yao pamoja na viapndo vyao ambavyo vitaathrikia na tathmini hiyo.

Sheha wa Shehia Tunguu Iddi Ramadhani Chumu amewahakikishia wananchi hao kuwa hakuna atakaedhulumiwa na tathmini hiyo mara baada ya kufanyika itarudisha mrejesho kwa wananchi.