Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

WAZIRI Wa Ardhi Na Maendeleo Ya Makaazi Mhe.Rahma Kassim Ali Ametoa Wito Kwa Wamiliki Wa Eka Za Serikali Ambao Walipewa Kwa Ajili Ya Matumizi Sahihi Ya Kilimo Kuacha Kuzitumia Eka Hizo Kinyume Na Matumizi Hayo

Mhe Rahma alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara zake ya kutembelea baadhi ya Eka Wilaya ya Magharibi A”na “B”ambapo imebainika kua kuna baadhi ya wenye Eka hizo huzikata viwanja na kuziuza kinyume na matumizi sahihi yaliwekwa na Serikali.

Aidha alifahamisha kua Wizara itahakikisha inazifatilia kwa makini Eka zote za Serikali na yoyote atakaekundulikana kwenda kinyume na matumzi sahihi ya Eka hizo hatua kali za kisheria zitachukuliwa zidi yake ikiwemo kunyanganywa.

“Tumefanya ziara kuzitembelea eka za Serikali na tumegundua kuna baadhi ya mashamba hayo yamekatwa viwanja na kuuziwa wananchi kinyume na utaratibu wa kisheria ambapo eka haitakiwi kuuzwa wala kubadilishwa matumizi hivyo yoyote Serikali imeamua kuzisimimia eka hizi kuona zinatumika kwa matumizi yaliyowekwa tokea awali na atakaebanikia basi tutachukua hatua za kumyang’anya”.alisisitiza Mhe.Rahma.

Aidha alifahamisha kua kwa yoyote ambae Alipewa EKa hizo ambae anataka kubadilisha matumizi Serikali imeweka utaratibu wa kuandika barua na Kuzifikisha Taasisi husika ambayo ni Wizara ya Ardhi na Wizara ikiridhia kua matumizi anayotaka kubadilisha yanakwenda sambamba mpango wa Serikali na sehemu husika basi hua hakuna pingamizi nasio kujiamulia mtu binafsi kubadilisha matumizi ambapo ni kosa la jinai.

“Wizara imeweka utaratibu unapotaka kubadilisha matumisi na inaangalia ni matumizi ya aina gani unataka kubadilisha ikiridhia basi na sio kujichukulia hatua mikononi mwako sio jambo la busara kabisa na hatutalifumbia macho.”alieleza Waziri huyo.

Hata hivyo aliwataka wananchi wanapotaka kununua viwanja kufika sehemu husika ambayo ni Kamisheni ya Ardhi kwa kujiridhisha kama sehemu hiyo haina mgogoro ili kuepuka kutapeliwa ambapo baadhi ya migogoro mengine ya ardhi husababishwa na madalali wasio rasmini kwa kuwauzia viwanya wananchi kinyume na utaratibu wa kisheria.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi Sleiman Haji Hassan amesema kua kwa sasa Kamisheni ya Ardhi imeazima kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote ambao wanajipatia fedha kwa njia isiyo rasmini kwa kuuza viwanja katika eka za Serikali ambapo ni kosa la jinai na atakaebainika atafikinishwa mahakamani pamoja na kunyanganywa eka aliyopewa.