Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mazingira rafiki kwa kuzifanyia marekebisho sheria zake ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Dkt. Mngereza Mzee Miraji ameeleza hayo katika mazungumzo maalum yaliowashirikisha ujumbe kutoka European Mortgage Federation na taasisi inayoshughulikia masuala ya mikopo ya ujenzi wa nyumba ya Dar es Salam (TMRC) wakati walipofika katika Afisi za Wizara ya Ardhi iliopo Maisara Jijini Zanzibar.
Katibu Mkuu Mngereza amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango yake kwa kuwakaribisha wawekezaji kuekeza katika ardhi ya Zanzibar huku sheria na sera masuala ya uwekezaji zikiwa zimeimarishwa.
Aidha, Dkt. Mngereza ameeleza kwamba dhamira ya ujumbe huo kutaka kufanya mkutano wa kimataifa Zanzibar ni dhamira njema na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makaazi itatoa kila aina ya ushirikiano katika kufanikisha azma hiyo.
Pia, Katibu Mkuu Mngereza ameueleza ujumbe huo uliofika Afisini kwake kuwa, dhamira yao ya kufanya mkutano wa kimataifa Zanzibar inakwenda sambamba na dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutaka kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kufanyia mikutano ya kimataifa ya kitalii.
“Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Mwinyi imedhamiria kuimarisha uchumi wake kwa kuanzisha utalii wa mikutano” Alisema Dkt.Mngereza
Amefafanua kwamba, Zanzibar imebarikiwa kuwa na fukwe nzuri pamoja na maeneo ya kihistoria jambo ambalo wageni watakaofika Zanzibar watafurahia kwa kuyatembelea maeneo hayo kwa kupata maelezo ya kihistoria.
Nae Katibu Mkuu wa Europian Mortgage Federation LUCA BERTOLT amesema wamekusudia kufanya mkutano wa kimataifa Zanzibar utakaowashirikisha wawekezaji kutoka nchi mbali mbali Duniani.
Katibu LUCA ameeleza kufanyika kwa mkutano huo hapa Zanzibar kutafungua fursa muhimu kibiashara kwa watu wa Zanzibar pamoja na kuitangaza nchi kimataifa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu kutoka taasisi ya (TMRC) kutoka Dar es Salam amesema kupitia mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Okotoba mwaka huu Zanzibar inaweza kupata wawekezaji ambao watajenga nyumba za bei nafuu huku ikiendelea kupendezesha mji wake kwa kuwa na majengo mazuri.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WAMM).
Januari 22, 2024.