Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi (WAMM) tarehe 03/04/2023 imesaini Hati ya Makubaliano na Kampuni ya Kitaifa ya Kijiografia na Misitu (IGN FI) ya Ufaransa kuhusu Mradi wa Taarifa za Usimamizi na Usaji wa Ardhi Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya hafla ya utiaji saini waziri dhamana wa wizara hiyo  Mhe. Rahma Kassim Ali amesema kufanya kazi kwa mfumo wa taarifa za Usimamizi na Usajili wa Ardhi utasaidia kwa kiasi kuondosha migogoro ya ardhi iliyokuwepo Zanzibar.

Waziri Rahma aliyasema hayo baada ya kushuhudia hafla ya utiaji saini ambapo ilifanyika Wizara Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Maisara Unguja. Alisema hatua hiyo ya utiaji saini ina manufaa makubwa hasa katika kuondoa migogoro ya ardhi ambayo inaonekana kujitokeza kila siku.

 “Tunaamini mfumo huo utasaidia sana kwani taarifa zitakuwa kwenye mfumo na mmiliki husika hasa wa ardhi atajulikana kwani taarifa za ardhi  zipo kwenye karatasi lakini mfumo sio rahisi kupoteza taarifa.” Alisema waziri huyo.

Waziri Rahma alisema hivi sasa wizara yake inaendelea na zoezi la utambuzi wa ardhi ambapo pia taarifa zake zitaingizwa katika mfumo na tayari wamefanya zoezi la utambuzi katika shehia 50 zimeshafanyiwa kazi na mategemeo ya Serikali ni kuitambua ardhi yote katika shehia 388 za Unguja na Pemba.

“Mfumo huu tuna matumaini makubwa kwamba migogoro ya ardhi mingi itaondoka na itakayokuwepo ni ile ya kawaida lile tatizo kubwa ambalo linatukumba wizara litaondoka kwa asilimia 95 na itakuwa manufaa makubwa ambayo Serikali ya awamu ya nane imepiga hatua kubwa.” Alifafanua Waziri Mhe Rahma kassim Ali .    

Hivyo alisema anaamini ndani ya mwezi mmoja upembuzi yakinifu wa mfumo huo utakuwa umeshakamilika na kwenda kwenye mfumo wenyewe hivyo ni matumaini yake ndani ya mwaka huu kabla ya 2024 mfumo huo utakamilika na kuanza kutumiwa rasmi.

Kwa upande wake  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Dk. Mngereza Mzee Miraji, alisema mfumo huo utakapoanza kazi utakuwa na faida kubwa ikiwemo ya kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa wawekezaji na wananchi, kupunguza urasimu na kutoa huduma rahisi ya kuaminika na salama kwa wateja kwani wananchi na wawekezaji wamekuwa wakitoa malalamiko katika jambo hilo. 

Alisema pia utapunguza muda wa kukagua, kusahihisha na kubadilisha ama kuhamisha umiliki wa ardhi kwa wananchi wawekezaji na miradi yote inayofanyika Zanzibar, kupunguza uvamizi wa ardhi, misitu, hifadhi za barabara na sehemu za wazi, uhifadhi wa ardhi na maliasili na kupunguza rushwa na viashiria vyote vya rushwa hasa ya ufatiliaji, usajili na uhamisho wa hatimiliki.

Mhandisi Dkt. Mngereza alibainisha kuwa utiaji saini huo ni mwanzo mpya ya kimapinduzi katika sekta ya ardhi nchini ambalo ndio lengo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuondoa urasimu na kuondoa migogoro ya ardhi hapa Zanzibar hivyo matumizi ya teknologia mpya ni njia moja ya kutatua changamoto zilizokuwepo katika suala la ardhi Zanzibar.

Mapema Mrajis wa Ardhi Dkt. Abdul-Nasser Hikmany alisema mfumo huo utasaidia kiutendaji pamoja na kutoa huduma bora kwa jamii kupitia Kamisheni ya Ardhi Zanzibar ambapo taasisi hiyo iko chini ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar.

Dkt Hikmany alisema malengo ya taasisi hiyo  kuwa taarifa zote ambazo zitahusu ardhi zitaingizwa katika mfumo huo ikiwemo utambuzi, mipango miji, usajili na mambo mengine ikiwemo maombi ya umiliki wa ardhi.

Alielezea kwamba mfumo huo sio mpya duniani  kwani umeshatumika katika nchi nyengine ikiwemo Uganda, Seralione na hata Tanzania bara ambao ufanya kazi kwa muda wa miaka mitano.

“Leo tumetia saini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kutekeleza upembuzi yakinifu ambayo itatuonesha gharama ya mfumo huu na utatengenezwa kwa jinsi ya mazingira ya Zanzibar yalivyo.” Alisema Dkt. Hikmany.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kijografia na Misitu (IGN FI) ya Ufaransa Christopher Dekeyne, alipongeza Serikali kufanya kazi pamoja na Taasisi yake kwani na wana uzoefu mkubwa katika mabara mengi hasa ya Afrika  wamefanikiwa na mradi huo na umeleta manufaa. Hivyo anaamini kwamba mfumo huo utaleta tija Zanzibar.

Alisema kazi hiyo itaanza kwa kufanya upembuzi yakinifu kujua mazingira ya Zanzibar na vitu vitakavyohitajika ili kuwa na mradi utakaokidhi haja na mahitaji ya Zanzibar na kuwezesha kutengeneza mfumo ambao utaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya kuinua uchumi wa Zanzibar.

Aidha alisema ni matumaini yake kwamba watapata ushirikiano wa kutosha ili kuweza kufanikisha mradi huo na kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.