Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Naibu Wziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Salha Mohammed Mwinyjuma amesema ziara za ufatiliaji wa Migogoro ya Ardhi ambayo huwasilishwa Wizarani kupitia Kamati ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ardhi zinalenga katika kujiridhisha ili kuweza kupata ufumbuzi wa kisheria bila kumdhulumu Mwananchi yoyote.

Ameyasema hayo huko Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja katika ziara zake za ufatiliaji wa Migogoro ya Ardhi ilioko Paje na Kizimkazi inayohusisha uvamizi wa maeneo kinyume na utaratibu wa makubaliano ya wahusika.

Aidha amesema kuwa Wizara kupitia Kamati ya Usuluhishi na utatuzi wa Migogoro ya Ardhi mara baada ya kupokea malalamiko ya Wananchi yanayohusiana na Migogoro ya Ardhi baina yao hufanya jitihada za kufika maeneo husika ili kuweza kuthibitisha juu ya kilichowasilishwa na baadae kutolea maamuzi.