Akizungumza katika ukumbi wa Makonyo, Chake Chake, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake kufuatia kuteuliwa tena kuingoza wizara hiyo, Mhe. Rahma alisema kuwa licha ya mafanikio makubwa ya kiutendaji yaliyopatikana katika kipindi kilichopita, bado kuna mapungufu yanayohitaji kushughulikiwa kwa dharura ili kufikia dira ya Serikali ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuweka alama ya mabadiliko katika sekta ya Ardhi na Makaazi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma, aliweka mkazo katika suala la uadilifu, akisema kuwa sekta ya ardhi inahitaji uwazi na uaminifu wa hali ya juu. Alisema ni muhimu kuondoa muhali katika masuala ya kiutendaji, hususan katika utatuzi wa migogoro ya ardhi Kisiwani Pemba, ambayo imekuwa changamoto inayoathiri ufanisi wa sekta hiyo. Aidha, alisisitiza kuimarishwa kwa Kamati ya Migogoro ya Ardhi ili kuongeza kasi ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndg. Khadija Khamis Rajab, aliwapongeza watendaji kwa utendaji uliosifiwa mara kwa mara, lakini akawahimiza kuendeleza ari na ushirikiano ili kufanikisha malengo ya wizara. Alibainisha kuwa serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili wizara hiyo.